History of the Church
HISTORIA YA PAROKIA YA MT. MARIA DE MATTIAS-MIVUMONI
Parokia ya Mt. Maria De Mattias-Mivumoni iko katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam na katika Dekania ya Mt. Gaspar del Bufalo. Parokia hii iko katika Manispaa ya Wilaya ya Kinondoni. Parokia hii inaendeshwa na Mapadre wa Jimbo.
Historia ya Parokia ya Mt. Maria De Mattias inaanzia pale ambapo Halmashauri ya Walei ya Kigango cha Mt. Fransisko Xaveri - Wazo Hill (Kwa sasa Parokia ya Mt. Benedikto Abate- Wazo Hill) ilipokabidhi uangalizi wa eneo hili la kanisa kwa Kanda ya Mt. Inyasi wa Loyola zikiwa na Jumuiya mbili za Mt. Inyasi wa Loyola na Mt. Martha mwezi Mei 2005. Wakati huo kulikuwa na hofu ya uvamizi wa viwanja kwani maeneo yalikuwa ni mapya na hivyo ramani ya eneo haikuwa ikifahamika vizuri. Jumuiya hizo mbili ziliendelea kuhudumia eneo hili kwa kufanya usafi, kupanda miti na kulinda mipaka kwa kushirikiana na Jumuiya nyingine zilizozaliwa baadaye. Mbali na shughuli hizo za uangalizi, sala za jumuiya, misa (zikiwemo za ubatizo na ndoa) na hata shughuli nyingine za kiroho zilifanyika katika eneo hili bila kuwa na jengo la kanisa.
Kutokana na umuhimu wa malezi ya kikristo kwa watoto na mafundisho mengine ya dini, mnamo mwezi Januari 2009 waamini waliamua kwa pamoja kujenga kibanda kidogo cha muda ambacho kingetumika kufundishia watoto mafundisho ya dini ifikapo mwezi Mei 2009. Hata hivyo, kwa sababu mbalimbali, ujenzi huo haukuweza kuanza hadi ilipofika mwezi Desemba 2009. Wakati huo, wazo liliibuka la kuwa na jengo dogo la kanisa badala ya kibanda cha kufundishia watoto.
Ujenzi wa jengo dogo la Kanisa ulianza rasmi mwezi Januari 2010 na ilipofika Aprili 2010 jengo lenye uwezo wa kukaa waamini 200 lilikuwa limefikia hatua ya kuwa na paa na hivyo kuruhusu ibada ya kwanza ya Pasaka kufanyika bila sakafu. Ujenzi wa jengo la Kanisa ulipitia hatua mbalimbali za usanifu na ramani ili kuendana na raslimali fedha zilizotakiwa kufanikisha kazi hii. Ujenzi huu uligharimu zaidi ya Shilingi Millioni Hamsini za Kitanzania (50,000,000.00), kiasi ambacho kinajumuisha michango ya fedha taslimu, vifaa vya ujenzi na nguvu kazi (gharama nyingine nyingi hazikuweza kukadiriwa kwa kuwa zilikuwa ni majitoleo kwa njia ya nguvu kazi, punguzo la bei ya vifaa n.k.). Ujenzi ulifanyika kwa kushirikisha jumuiya zote na ulihusisha kujenga sakristia, ofisi, vyoo, kuweka nguzo za uzio, kununua vifaa mbalimbali mfano viti, meza, kabati n.k.
Baada ya ujenzi kukamilika kwa asilimia kubwa, kanisa lilipata hadhi ya kuitwa kigango. Hivyo uzinduzi rasmi ulifanyika tarehe 29 Agosti 2010 na Baba Padre Felix Mushobozi, Katibu wa Shirika la Damu Takatifu ya Yesu Duniani chini ya uongozi wa Parokia ya Damu Takatifu ya Yesu Tegeta na Baba Paroko akiwa Padre Richard Tiganya. Ili kuweza kuendelea na majukumu mbalimbali ya kigango wajumbe wa Kamati Tendaji na baadhi wa Vyama vya Kitume ngazi ya Parokia na Kamati ya Ujenzi waliteuliwa, kusimikwa na kuanza kazi rasmi wakati wa misa hiyo ya uzinduzi. Mara baada ya uzinduzi Padre Josephat Msuya alichukua nafasi ya Paroko baada ya Padre Richard Tiganya kuhitajika masomoni ulaya ya muda mrefu. Wakati huo, Kigango kilikuwa na jumla ya jumuiya nane ambazo ni Mt. Inyasi wa Loyola, Mt. Martha, Mt. Rita wa Kashia, Mt. Monika, Mt. Katarina wa Siena, Mt. Ambrose, Mt. Lusia na Mt. Thomas Mtume.
Hapo awali kabla ya Parokia, Kigango kiliwekwa chini ya Mt. Monika kama Msimamizi Somo wake. Baadaye ilionekana ni muhimu kubadilisha Msimamizi Somo wa Kigango ili kuondokana na mkanganyiko ambao ulikuwa unatokana na jina la Mtakatifu huyo kutumiwa na baadhi ya Parokia na Vigango vingine vya Jimbo. Kutokana na maelekezo kutoka kwa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, kuanzia tarehe 28 Agosti, 2013 Kigango kiliwekwa rasmi chini ya Mt. Maria De Mattias kama Msimamizi Somo wake hadi sasa.
Ziara iliyofanyika kigangoni mnamo Januari 2014 na Mhashamu Baba Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Eusebius Nzigilwa pamoja na mambo mengine ilikuwa na lengo la kutathmini maendeleo ya jumla na vigezo vya kuwezesha Kigango kuwa parokia. Kigezo kimojawapo katika tathmini hiyo ilikuwa uwepo wa nyumba ya mapadre. Baada ya ziara hiyo kanisa lilipata hadhi ya kuitwa Parokia terehe 7 Julai 2014 na kukabidhiwa kwa utume wa Mapadre wa jimbo na Padre Edwin Epimack Kigomba ndiye Paroko wa kwanza hadi sasa na Msaidizi wake alikuwa Padre Paul Sabuni Mboje.
Makabidhiano rasmi ya Parokia yalifanyika mwezi Agosti 2014 na Padre Novatus Mbaula, Mkurugenzi wa Msimbazi Centre.Wakati huo, Parokia ilikuwa na jumla ya jumuiya 13. Baada ya kutangazwa Parokia, Kigango cha Mt. Benedikto Abate –Wazo Hill kilikabidhiwa chini ya uongozi wa Parokia ya Mt. Maria De Mattias kikiwa na jumuiya 23 hivyo kufanya jumla ya jumuiya kufikia 36. Baadae jumuiya 22 ziliongezeka; 13 kutoka Mt. Benedikto Abate-Wazo na 9 kutoka Mt. Maria De Mattias-Mivumoni hivyo kufikia jumuiya 58. Hata hivyo, baada ya Parokia Teule ya Mt. Benedikto Abate –Wazo kutangazwa Parokia kamili Julai 2016, Parokia ya Mt. Maria De Mattias –Mivumoni ilibaki na jumuiya 22 na ziliendelea kuongezeka.
Parokia ya Mt. Maria De Mattias –Mivumoni ina jumla ya waamini 2,618 ambapo watoto ni 970, Vijana 337 Akina baba 562 na akina mama 645 kulingana na taarifa ya 2018. Kwa sasa Parokia inafamilia 678 na Jumuiya Ndogondogo za Kikristo 31 nazo ni Jumuiya ya Mt. Inyasi wa Loyola, Jumuiya ya Mt. Martha, Jumuiya ya Mt. Rita wa Kashia, Jumuiya ya Mt. Monika, Jumuiya ya Mt. Katarina wa Siena, Jumuiya ya Mt. Ambrose, Jumuiya ya Mt. Thomas Mtume, Jumuiya ya Mt. Lusia, Jumuiya ya Mt. Gaspare del Bufalo, Jumuiya ya Mt. Kizito, Jumuiya ya Mt. Augustino, Jumuiya ya Mt. Anna, Jumuiya ya Mt. Margareta Maria Alakok, Jumuiya ya Mt. Yohane Paulo II, Jumuiya ya Mt. Teresia wa Mtoto Yesu, Jumuiya ya Mt. Yohane wa XXIII, Jumuiya ya Mt. Josephine Bakhita, Jumuiya ya Mt. Anthony wa Padua, Jumuiya ya Mt. Marko Mwinjili, Jumuiya ya Mt. Luka Mwinjili, Jumuiya ya Mt. Yosefu Mfanyakazi, Jumuiya ya Mt. Maria Goreti, Jumuiya ya Mt. Marcelino, Jumuiya ya Mt.Veronica, Jumuiya ya Mt. Joakimu, Jumuiya ya Mt. Yohane Bosco, Jumuiya ya Mt. Petro, Jumuiya ya Familia Takatifu, Jumuiya ya Mt. Mikael Malaika Mkuu Jumuiya ya Mt. Yuda Tadei na Jumuiya ya Mt. Martini De Porres.
Takwimu za sakramenti kuanzia 2010 hadi Juni 2018
Mwaka
|
Ubatizo-Watoto |
Komunio
|
Kipaimara |
Ndoa
|
Ubatizo Watu Wazima |
Wakristo waliopokelewa ukatoliki |
2010 |
24 |
0 |
0 |
6 |
1 |
0 |
2011 |
47 |
17 |
21 |
8 |
3 |
0 |
2012 |
55 |
39 |
23 |
10 |
10 |
0 |
2013 |
75 |
29 |
32 |
5 |
5 |
0 |
2014 |
34 |
36 |
34 |
5 |
6 |
5 |
2015 |
95 |
25 |
19 |
6 |
48 |
5 |
2016 |
93 |
81 |
86 |
23 |
9 |
3 |
2017 |
66 |
106 |
82 |
15 |
12 |
4 |
2018 |
55 |
83 |
63 |
12 |
6 |
11 |
Vyama vya Kitume vilivyopo katika Parokia ni pamoja na WAWATA (562), UWAKA (485), Vijana (226), Utoto Mtakatifu (562), Moyo Mtakatifu wa Yesu (7), Legio Maria (8), Wadiministranti (36), Shikwaka (86) (Kwaya ya Mt. Maria De Mattias, Kwaya ya Mt. Yohane Paulo II, Kwaya ya Kristo Mfalme) na Kwaya ya Watoto. Uongozi wa Halmashauri Walei ya Parokia kuanzia 2012 hadi 2018
Mwaka 2012 hadi 2015
|
||
Na. |
Jina |
Wadhifa |
1
|
Ndg. Cosmas Mwaisobwa
|
Mwenyekiti
|
2
|
Ndg. Chrysanthus Chenga
|
Makamu M/kiti
|
3
|
Ndg. Adelaide Sallema
|
Katibu
|
4
|
Ndg. Andrew Peter
|
K/Msaidizi
|
5
|
Ndg. Mary Mwapili
|
M/Hazina
|
Mwaka 2015 hadi 2018
|
||
Na. |
Jina |
Wadhifa |
1
|
Ndg. Chrysanthus Chenga
|
Mwenyekiti
|
2
|
Ndg. Zephrine Galeba
|
Makamu M/kiti
|
3
|
Ndg. Adelaide Sallema
|
Katibu
|
4
|
Ndg. Andrew Peter
|
K/Msaidizi
|
5
|
Ndg. Mary Mwapili
|
M/Hazina
|
Ee Mtakatifu Maria De Mattias, mtangazaji na mtume hodari wa Damu Takatifu ya Yesu. Uliyetumia maisha yako yote kwa kuvuta roho za watu kwenye chemchemi ya neema inayotoka moyoni mwa Yesu Msulubiwa. Unijalie moto wa mapendo kama ule uliogusa moyo wako na bidii kwa wokovu wa watu, uliokuwa lengo kuu na la pekee la maisha yako. Amina.